Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu imesema kuwa haihusiki kumtafutia
mnufaika wa mkopo ajira badala yake inahusika kumpatia mwanafunzi mkopo
na akishamaliza muda wa masomo atatakiwa kurejesha mkopo wake.
Hayo yamesemwa jana Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Msaidizi wa
Habari, Elimu na Mawasiliano kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu
Cosmas Mwaisobwa wakati akijibu maswali ya wananchi kupitia kipengele
cha Kikaango cha EATV.
“Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu inatoa mikopo suala la kutafuta ajira
halituhusu hivyo mnufaika yoyote asiwe na kigezo kwamba hajapata kazi ,
hiyo siyo kazi yetu, kazi yetu ni kuwawezesha kupata elimu basi” Alisema
Mwaisobwa.
Aidha Mwaisobwa alisema wanufaika wote ambao walipata mikopo wanatakiwa
kukatwa asilimia 8% ya pato la mwezi, na kama mtu anafanya kazi binafsi
na hakatwi popote atatakiwa kutoa kiwango cha 120,000/= na kwa ambao
wamenufaika na hawataki kuanza kulipa mkopo watapigwa penati ya 10% ya
mkopo kwa mwaka.
Pamoja na hayo Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu imewataka walioomba mikopo
kuvuta subira kwani Bodi inasubiri majina kutoka Tume ya Vyuo Vikuu ili
Bodi ya Mikopo iweze kufahamu vyuo walivyopangiwa na kiwango cha ada
ili haki iweze kutendeka kwa waombaji.

No comments:
Post a Comment