Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndulu jana alitolea
ufafanuzi hali ya kiuchumi nchini huku akieleza siri ya kilio
kinachovuma cha fedha kupotea mtaani na nyingine zikidaiwa kufichwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Profesa
Ndulu alisema kuwa kwakuwa taasisi hiyo ndiyo inayofahamu fedha zote
zilizopo benki na zilizopo mtaani, inafahamu kuwa hakuna fedha
iliyopotea bali fedha zimepotea kwa watu waliokuwa wanazipata kwa njia
ya udanganyifu kwakuwa sasa Serikali imebana mianya hiyo.
“Hakuna fedha iliyopotea, Serikali imebana shughuli za watu na ‘mission
town’ sasa shughuli zote zinafanywa na Serikali. Hivyo, kwao fedha
zimepotea, lakini kwetu hazijapotea,” alisema Profesa Ndulu.
Hata hivyo, Profesa Ndulu alikiri kupungua kwa fedha katika mabenki
nchini hali iliyopelekea kupunguza kasi ya utoaji mikopo kwa wananchi.
Alisema hali hiyo ilitokana na kuhamishwa fedha za mashirika ya umma na
taasisi kutoka benki za biashara kwenda BoT.
“Fedha hizo zitarudi katika benki hizo wakati zitakapopelekwa kwenye
Halmashauri kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali,” Profesa Ndulu
aliahidi.
Katika hatua nyingine, Gavana huyo wa Benki Kuu alisema kuwa uchumi
unatarajiwa kukuwa kwa asilimia 7.2 mwaka huu, huku akibainisha kuwa
moja kati ya sababu zinazopelekea ukuaji huo ni ongezeko la uzalishaji
wa umeme na saraju.
Akizungumzia hali ya deni la taifa, alisema kuwa deni la taifa la ndani
limeongezeka kutoka shilingi trilioni 8.6 Mwezi Desemba mwaka jana hadi
shilingi trilioni 10 mwezi Juni mwaka huu.
Profesa Ndulu alibainisha kuwa wakati deni linalotokana na kukopa ndani
likipaa, deni linatokana na ukopaji wa limepungua baada ya Serikali
kupunguza ukopaji nje ya nchi.

No comments:
Post a Comment