WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ametoa waraka akisema kitendo cha
askari wa Jeshi la Polisi kuwakamata wakati wakiwa kwenye kikao cha
ndani cha Chadema jana kimemuimarisha na kumpa nguvu zaidi ya kudai
demokrasia.
Katika waraka wake kwa vyombo vya habari leo, Lowassa amesema
anafurahishwa na kutiwa moyo na jinsi Watanzania walivyoipokea
operesheni yao ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta) iliyopangwa
kuanza kesho kwa maandamano na mikutano, lakini vitendo vya polisi
vinawapa wasiwasi wananchi.
Lowassa, akiwa na Freeman Mbowe, ambaye ni mwenyekiti wa Chadema, John
Mnyika (naibu katibu mkuu-Bara) na viongozi wengine wa chama hicho kikuu
cha upinzani walikamatwa jana wakiwa kwenye kikao cha ndani
kilichofanyika Hoteli ya Girrafe na baadaye kwenda kituo kikuu cha
polisi kwa mahojiano kabla ya kuachiwa na kutakiwa kwenda kituo hapo
kesho.

No comments:
Post a Comment