Agosti 22, 2016 Umoja wa Vijana wa CCM tuliutangazia umma na dunia
kwamba ifikapo Agosti 31 mwaka huu tutaitisha maandamano ya amani nchi
nzima yenye lengo la kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Magufuli kwa utendaji wenye tija,
ufanisi na uliorudisha imani na matumaini kwa wananchi.
Msimamo na dhamira ya kufanya maandamano hayo ya amani yenye maudhui na
kusudio hilo, bado uko pale pale ingawaje si kwa tarehe tuliopanga na
kutangaza awali yaani Agosti 31 mwaka huu.
Jumuiya yetu kama mjuavyo ni ya Vijana wa CCM, (UVCCM) inapata malezi
kwa karibu mno na Jumuiya ya Wazazi ya CCM. Wiki ya jana Mwenyekiti wa
Wazazi Taifa Nd. Abdallah Bulembo alikutana na waandishi wa habari
akitutaka UVCCM tuahirishe maandamano ya Agosti 31 mwaka huu hadi wakati
mwingine.
Kwa mujibu wa Katiba ya Chama Cha Mapinduzi, Jumuiya ya Wazazi ndiyo
Msimamizi wa Malezi, Maadili na Adabu kwa Vijana wote nchini, sisi UVCCM
tunaamini kuwa sikio halishindani na kichwa, mtoto ni mtoto kwa Wazazi
wake hakui, hana jeuri wala ubishi.
Mtoto au watoto wanaokaidi amri, ushauri au maelekezo ya Wazazi wao
huitwa watukutu, wenye viburi, manunda na wasioambilika. UVCCM si
watukutu, hatukufunzwa tuwe wabishi, wakaidi na wenye viburi.
Tumezingatia kutii maelekezo, makatazo na maonyo , tumeambiwa tuahirishe
maandamano yetu nasi tumekubali na kuheshimu mambo tuliyoaswa.
Sambamba na hilo tumepata majibu ya barua yetu tuliyomwandikia Mkuu wa
Jeshi la Polisi nchini (IGP Ernes Mangu) inayotutaka tuache kufanya
maandamano yetu kwa sababu Polisi wamezuia mikutano ya hadhara ya Vyama
vya Siasa na maandamano nchi nzima.
Jambo jingine ambalo limetufanya pia tuahirishe maandamano yetu ya Amani
ni taarifa ya kintelejinsia iliowasilishwa na Kamati yetu ya Usalama na
Maadili ya UVCCM mbele ya kikao cha Sekreteriet yetu, nayo ilipendekeza
suala hilo liahirishwe kwa wakati huu hadi muda mwingine.
Pia jambo jingine ambalo limefanya maandamano hayo tuyabatilishe ni
kulipisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ ) ambalo litakuwa katika
shughuli za maadhimisho miaka 52 tokea kuanzishwa kwake.
Wanajeshi wetu watakuwa katika kazi mbalimbali za kijeshi kwenye kambi
zao na mitaani kufanya usafi wa mazingira, hivyo isingependeza na wala
si heshima wakati sisi tukiandamana, wao wakifanya kazi muhimu kila
mmoja wetu zinazomgusa badala yake ni vyema kuwaunga mkono jambo
wanalolifanya la usafi wa mazingira.
UVCCM tumekubali, hatutaki kuingia katika uvunjaji wa sheria hasa baaada
ya kutakiwa kuahirisha na mamlaka za Kisheria hadi wakati mwingine
muafaka na si wakati huu.
Tunaelewa kwamba uamuzi wetu wa awali wa kutaka kuandamana kwa amani
hata kama tungenyimwa kibali ungetugharimu, ungetusababishia madhara na
pengine hasara, kwa wakati huu na kuona jambo lenyewe ni la kuipa Ari
serikali katika kuhimiza Uwajibikaji, Utendaji na Usimamizi bora wa
Uendeshaji wa masuala ya kiutawala.
Tulishusha maagizo kwa Makatibu wetu wote wa Mikoa yote 32 na Wilaya 171
ya Kichama tukiwataka waandike barua katika Ofisi za Ma RPC na OCD,
washirikiane ili kuratibu maandamano na kuyafanikisha kama
tulivyokusudia.
Watendaji wetu wa ngazi husika wamefuata maelekezo, wametii taratibu
zetu za kiutendaji na leo tumewajulisha tena wasitishe maandamano hadi
tutakapowapa tena maelekezo mengine. Tunawahimiza na kuwataka ni vyema
kutii mamlaka za Kikanuni na Kisheria.
UVCCM kwa wakati huu tumeamua kuachana na maandamano badala yake
tunajikita katika matayarisho ya kuwapeleka Vijana wetu wakashiriki
katika Mafunzo ya Siasa, Utawala, Uongozi, Ufundi na Ujasiriamali
yatakayoanza kufanyika katika Chuo chetu kilichopo huko Ihemi Mkoani
Iringa ambapo kitakuwa kielelezo na alama nzuri ya kumuunga mkono
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kwa vitendo.
Tumewataka Makatibu wetu wa Mikoa na Wilaya kuendelea na zoezi la
Uratibu na Uhakiki kwa Vijana ambao watateuliwa kushiriki Mafunzo hayo
huko Ihemi.
UVCCM tunarejea kusema tena kwamba dhamira ya maandamano yetu ya kusifu
Utendaji wa Serikali ya awamu ya tano iko pale pale ila tutapanga tarehe
nyingine katika wakati ujao badala ya kufanyika Agosti 31 mwaka huu
kama tulivyotangaza hapo awali.
UVCCM tunawataka Vijana wote kuendelea kuheshimu Tunu ya Amani Umoja na Mshikamo wetu kwa Taifa.

No comments:
Post a Comment