TAMKO
la Tundu Antipas Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), akilitaka Jeshi la Polisi kuacha kuwashikilia watu
10 waliokamatwa kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo uchochezi, limeanza
kutekelezwa kwa shingo upande, anaandika Faki Sosi.
Jumamosi
iliyopita, Lissu alilitaka jeshi hilo kuacha kuvunja Katiba na Sheria
za nchi kwa kuwashikilia watuhumiwa hao zaidi ya wiki mbili badala ya
kuwafikisha mahakamani ndani ya masaa 48, kama sheria zinavyoelekeza.
“Tunalitaka
Jeshi la Polisi kuwafikisha watuhumiwa hao mahakamani siku ya Jumanne
ya wiki ijayo la sivyo tutalifikisha jeshi hilo mahakamani ili
likajieleza kwa uvunjifu wa Sheria na Katiba,” alisema Lissu katika
tamko lake jumamosi ya wiki iliyopita.
Baada
ya tamko hilo la Lissu, Jeshi la Polisi lilianza kuwasafirisha
watuhumiwa liliowakamata mikoa mbalimbali na kuwaleta Dar es Salaam.
Siku
ya juzi jeshi hilo liliwasafirisha watuhumiwa Ignasia Mzenga wa
Morogoro na Alex John wa Dodoma ili kuwarudisha katika mikoa
waliyokamatiwa huku Mdude Nyagali na wenzake watatu wakisafirishwa
kwenda Mkoa wa Songwe siku ya jana.
Jijini
Dar es Salaam polisi imewafikisha mahakamani mahabusu watano miongoni
mwa kumi iliokuwa ikiwashikilia, hata hivyo waendesha mashitaka wa
serikali hawakuandaa hati ya mashitaka ya watu hao na hivyo kusababisha
kutopandishwa kizimbani.
Kufuatia
kitendo hicho, Lissu ameiambia MwanaHALISI Online kuwa waendesha
mashtaka wa serikali wamefanya roho mbaya na uzembe wa makusudi
kutoandaa mashitaka ya watu hao licha ya kuwashikilia kwa muda wa siku
20.
“Haiwezekani
kukaa na watuhumiwa kwa siku 20 halafu leo wanakuja mahakamani bila ya
kuwa na hati ya mashtaka, ina maana walikuwa hawajui wanataka
kuwafungulia kesi gani? Huu ni uzembe mkubwa kwa serikali hii na
waendesha mashitaka wake,” amesema Lissu.
Lissu
ameeleza zaidi akisema, “tulitegemea watu hawa wapandishwe kizimbani
leo lakini hali imekuwa tofauti, serikali imeshindwa kuandaa hati ya
mashitaka kwa makusudi na kwa kweli dhamira yetu ya kufungua kesi ya
kulishtaki Jeshi la Polisi na serikali ipo pale pale.”

No comments:
Post a Comment