Serikali imeendelea kupigwa mweleka katika kesi ya uchochezi dhidi ya
mshitakiwa Tundu Lissu baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutupa
pingamizi la Wakili wa Serikali wakitaka wakili Peter Kibatala kujitoa
kumtetea mwanasiasa huyo.
Lissu, ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema
alipandishwa kizimbani Agosti 5, na kusomewa mashtaka matatu, mawili
kati yake yakiwa ni ya uchochezi na moja la kuidharau mahakama.
Pigo la kwanza la upande wa mashtaka ni pale Lissu alipopangua hoja na
kufanikiwa kupata dhamana, wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani kwa
mara ya kwanza.
Jana ilikuwa ushindi mwingine kwa upande wa utetezi, baada ya Mahakama
kutupa pingamizi la upande wa mashtaka lililotaka Kibatala ajitoe katika
jopo la mawakili wanaomtetea Lissu.
Upande wa mashtaka ulioongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja
Nchimbi, uliweka pingamizi hilo kwa maelezo Kibatala ni shahidi wao kwa
kuwa alikuwapo siku na mahali wakati Lissu akitoa maneno yanayodaiwa ya
uchochezi.
Wakili Kibatala ambaye ni kiongozi wa jopo la mawakili wanaomtetea
Lissu, alipinga hoja za Serikali za kutaka ajitoe katika kesi hiyo,
mvutano ambao ulisababisha kesi hiyo kuahirishwa mara mbili.
Wakili Kibatala alipinga kuwa hakuna kifungu cha sheria kinachomzuia
wakili kumtetea mteja wake kwa sababu tu ya kushuhudia akitoa maelezo
yake Polisi.
Akitoa uamuzi wa pingamizi hilo la Serikali, Hakimu Mkazi Mfawidhi,
Cyprian Mkeha anayesikiliza kesi hiyo, hakukubaliana na hoja za upande
wa Jamhuri (mashtaka) na hivyo akalitupa pingamizi hilo.
Hakimu Mkeha alikubaliana na hoja za wakili Kibatala kuwa hakuna kifungu chochote cha sheria kinachomzuia kumtetea Lissu.
Alisisitiza kuwa Kibatala ataendelea kuwa wakili wa Lissu katika kesi
hiyo na kwamba kama upande wa mashtaka ukimhitaji awe shahidi wao
utalazimika kumuomba. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 19.

No comments:
Post a Comment