RAIS John Magufuli, amemtaka Dk. Ali Mohamed Shein, kumpa tuzo Jecha
Salim, mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Zanzibar, kutokana na kile
alichokiita kazi nzuri aliyoifanya visiwani humo mwaka jana, kwa kufuta
matokeo ya uchaguzi mkuu.
Rais Magufuli aliyasema hayo jana jioni, katika ziara yake ya kikazi
visiwani Pemba. Wakati Rais Magufuli akichaguliwa katika uchaguzi wa
Oktoba mwaka jana, Dk. Shein alichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar kufuatia
uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi mwaka huu.
“Nampongeza sana Jecha kwa kazi nzuri aliyofanya kwa mujibu wa Katiba ya
Zanzibar, na kwa kweli Dk. Shein kama kuna tuzo zako utakazotoa,
naomba usimsahau kumpa na Jecha,” alisema Rais Magufuli.
Rai Magufuli pia alimtaka Rais huyo wa Zanzibar kumtaarifu yeye ili
awashughulikie watu wote wanaomsumbua visiwani humo au wanaoonekana
kumzidi nguvu.
“Rais Shein kama kuna mtu unaona anakusumbua wewe au anakupa tabu
nijulishe mimi tu, hata dakika tano hazitapita nitamshughulikia,”
ameeleza.
Kauli hiyo inakuja, ikiwa ni zaidi ya miezi kumi sasa tangu hali ya
mahusiano baina ya wananchi wa Zanzibar iwe tete, tangu pale Jecha Salim
Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi visiwani humo (ZEC) alipotangaza
kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Mahusiano hayo mabaya yamesababisha, wafuasi wa vyama vya CUF na CCM
vyenye nguvu zaidi visiwani humo, kufikia hatua ya kusitisha ushirikiano
katika shuguli za kiuchumi na kijamii ikiwemo kutohudhuria misiba na
kutonunua bidhaa za mtu wasiyeendana naye kiitikadi.
“Niombe vyombo vya ulinzi na usalama wafuatilie hao wanaokatakata na
kuchoma karafuu washughulikiwe bila huruma. Atakayejaribu kuichezea
amani, atacheza yeye tena mchezo asiojua kuucheza,” aling’aka Rais
Magufuli.
Tangu kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka jana visiwani Zanzibar, hali ya usalama imekuwa si ya kuridhisha.
Nyumba na mashamba ya karafuu yamekuwa yakichomwa moto, huku baadhi ya watu wakitiwa mbaroni na vyombo vya dola kwa tuhuma hizo

No comments:
Post a Comment