Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi amefariki dunia. Akiwa na miaka 96, Jumbe
aliishi muda mrefu sana kwa kigezo chochote kile. Alikuwa mwasisi wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mara baada ya Mapinduzi ya January 1964.
Alikuwa pia mwasisi wa Muungano ulioizaa Tanzania miezi michache baadae.
Baada ya Sheikh Abedi Amani Karume kuuawa mwezi April 1972, Jumbe
aliteuliwa kuwa Rais wa Pili wa Zanzibar, na alishikilia madaraka hayo
hadi January 1984. Wasomi wa Muungano wameandika kwamba wakati Karume
anauawa mahusiano yake na Mwalimu Nyerere yalikuwa yameharibika kiasi
kwamba Jumbe (kwa upande wa Zanzibar) na Bhoke Munanka (kwa upande wa
Tanganyika) ndio walikuwa kiunganishi cha mawasiliano kati ya Mwalimu na
Karume. Hii pengine ndio sababu Mwalimu alitumia ushawishi wake
kuhakikisha Jumbe anateuliwa kumrithi Karume.
Hata hivyo, Jumbe atakumbukwa zaidi na historia kwa upinzani wake kwa
mfumo wa sasa wa Muungano kuliko, pengine, kwa jambo jingine lolote.
Jumbe alikuwa mwanasiasa wa kwanza, baada ya era ya Karume, kutambua
kwamba muundo wa serikali mbili ulikuwa umeipokonya Zanzibar mamlaka
yake na kuyahamishia Tanganyika. Alikuwa wa kwanza kutambua kwamba
kuzaliwa kwa CCM, katika context ya Muungano, kulimaanisha mwisho wa
mamlaka yaliyokuwa reserved kwa Zanzibar chini ya Makubaliano ya
Muungano ya mwaka 1964.
Sio tu alitambua bali pia Jumbe alichukua hatua kupinga Zanzibar
kupokonywa mamlaka yake hayo. Ili kufanikisha azma yake, Jumbe
alilazimika kumwachisha kazi Mwanasheria Mkuu wake aliyepewa na Mwalimu
Nyerere, Damian Lubuva, na kumwajiri Bashir Ebassuah Kwaw Swanzy, raia
wa Ghana, kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar. Kwaw Swanzy ndiye
aliyeandaa 'hati ya mashtaka' dhidi ya Muungano iliyokamatwa na watu wa
usalama wa Mwalimu na baadae kutumika kumsulubu Jumbe kwenye kikao cha
NEC ya CCM Dodoma January 1984.
Kwa sababu ya upinzani huo, Jumbe aling'olewa madarakani pamoja na
Waziri Kiongozi wake Ramadhani Haji Faki na Mwanasheria Mkuu Kwaw Swanzy
alitangazwa persona non grata na kufukuzwa nchini. Mwalimu akatangaza
'kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa' Zanzibar na waZanzibari wengi
wapinzani wa Muungano, kama Mwanasheria Mkuu wa kwanza Wolfgang Dourado,
kuwekwa kizuizini.
Miaka kumi baada ya kuondolewa madarakani, Alhaj Aboud Jumbe alichapisha
kitabu chake juu ya Muungano, 'Miaka Thelathini ya Dhoruba', ambako
aliweka bayana ugomvi wake na Mwalimu juu ya Muungano. Jumbe ni kiongozi
pekee wa juu wa rika la wapigania uhuru wa Tanzania kuandika memoirs
zake juu ya Tanzania na matatizo ya Muungano wake. Hata Mwalimu
hakufanya hivyo na alikufa na siri zake juu ya mambo mengi makubwa
yalitokea wakati wa utawala wake.
Kwangu mimi, hii ndio merit kubwa na mchango mkubwa wa Alhaj Aboud Jumbe
kwa kizazi cha sasa na vijavyo vya waTanzania. Alikuwa na ujasiri wa
kusema na kuandika juu ya 'The Forbidden Subject', tena katika kipindi
cha Mwalimu Nyerere ambapo ujasiri wa aina hiyo ulikuwa ni jambo la
hatari kubwa. Kwa sababu hiyo hiyo, Jumbe alilazimika kuishi theluthi ya
mwisho ya maisha yake 'kifungoni' Mji Mwema, Kigamboni, ambako
alipelekwa mara baada ya kung'olewa madarakani mwaka '84.
Sikuwahi kubahatika kuonana na Alhaj Aboud Jumbe wakati wa uhai wake.
Hata hivyo, nimejifunza mengi sana kutoka kwake, hasa ujasiri wa kuuhoji
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Jumbe amekuwa na ushawishi mkubwa
sana kwenye mjadala wa Muungano kwa zaidi ya miongo mitatu sasa.
Ninadiriki kusema kwamba hoja ya Serikali Tatu ilianzia kwa Jumbe.
Roho, spirit, yake ilikuwa kila mahali wakati wa mchakato wa Katiba Mpya
kati ya 2011 na 2014. Kivuli chake kilikuwa kila mahali wakati wa Bunge
Maalum la Katiba mwaka 2014. Pengine kuliko hata Mwalimu Nyerere, Jumbe

No comments:
Post a Comment