Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeongeza nguvu kwa
kutuma askari wengine 80 katika oparesheni ya kusaka majambazi
inayoendelea katika maeneo ya Vikindu, wilayani Mkuranga mkoani Pwani.
Akizungumza na vyombo vya habari leo katika kituo kikuu cha Polisi Dar
es Salaam, Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo Kamishna Simon Sirro, amesema
Jeshi hilo limeanza rasmi oparesheni hiyo usiku wa kuamkia jana, ikiwa
na lengo kusaka watu wanaoshukiwa kuwa ni majambazi wanaodaiwa kufanya
matukio kadhaa ya ujambazi likiwemo lile la kuuawa kwa askari wanne
waliokuwa wakienda lindoni, katika benk ya CRDB, Mbade jiji Dar es
Salaam.
Amesema kuwa katika oparesheni hiyo kuna watu waliouawa na wengine
wanashikiliwa na jeshi hilo, lakini amekataa kutaja idadi yoyote ile ya
waliouawa au waliokamatwa kwa sababu za kiusalama kwa kuwa oparesheni
hiyo bado inaendelea.
Kuhusu taarifa za uwepo wa askari aliyeuawa, Kamishna Sirro amekataa
kuthibitisha au kukanusha na kusema kuwa taarifa kamili kuhusu
oparesheni hiyo itatolewa siku ya Jumanne ya wiki ijayo.
Amewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu, na kutoa ushirikiano kwa
jeshi hilo kwa kutoa taarifa zitakazoweza kufichua wahalifu hao na
kusisitiza kuwa jeshi hilo litawabaini na kuwatia nguvuni wote
waliohusika.
Katika hatua nyingine, Sirro ameendelea kupiga marufuku maandamano ya
aina yoyote yale katika mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya zuio
la jeshi la polisi la kupiga marufuku mikutano ya kisiasa na maandamano
nchi nzima.
Usiku wa kuamkia jana, hali ya taharuki iliwakumba wakazi wa Vikindu
baada ya kikosi maalum cha askari kuvamia nyumba moja iliyoko eneo hilo,
na kisha kuzuka kwa majibizano ya risasi kati ya polisi na wanaodaiwa
kuwa ni majambazi waliokuwa katika nyumba hiyo.

No comments:
Post a Comment