SAKATA la Dk. Emmanuel
Nchimbi, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Umoja wa Vijana wa Chama
Cha Mapinduzi (UVCCM), kuhusishwa na uuzaji ‘kiholela’ wa viwanja 200
mali ya jumuiya hiyo, limechukua sura mpya, anaandika Charles William.
Agosti 16, mwaka huu,
James Rock Mwakibinga, kada maarufu wa UVCCM, alijitokeza na kukitaka
chama chake kiwachukulie hatua kali baadhi ya viongozi wa kitaifa ndani
ya umoja huo ambao wameshiriki vitendo vya ufisadi wa mali za chama,
akiwemo Dk. Nchimbi.
“Kuna maeneo mengi
ambayo Baraza Kuu halikuyagusa katika kikao hicho, mfano; hawakugusia
vile viwanja 200 vya Temeke ambavyo vimeuzwa kinyemela na Dk. Nchimbi na
kwa sasa vimebakia vinne tu,” alisema.
Mwakibinga alikuwa
akizungumzia kutokuridhishwa kwake na hatua za kinidhamu zilizochukuliwa
na Baraza Kuu la UVCCM kwa watuhumiwa wa ubadhirifu wa mali za jumuiya
hiyo, ambapo alidai kuwa, baadhi ya vigogo akiwemo Nchimbi wameachwa.
Ikiwa ni zaidi ya wiki
moja sasa tangu Nchimbi kutuhumiwa, hatimaye amejitokeza na kueleza
kusudio lake la kumfikisha Mwakibinga mahakamani kwa madai ya kumchafua
kupitia tuhuma alizotoa.
Barua iliyoandikwa
kupitia kampuni ya uwakili inayojulikana kama FK imesema, “sisi ni
mawakili tunaoandika barua hii chini ya maelekezo ya Dk. Emmanuel
Nchimbi (mteja wetu).
“Katika kikao chako na
waandishi wa habari (16 Agosti mwaka huu), ulitoa tuhuma nyingi na nzito
dhidi ya mteja wetu na uongozi mzima wa UVCCM ambapo ulitamka pamoja na
mambo mengine tuhuma za kubuni ambazo haukuwa na uhakika nazo wala
uthibitisho wake.”
Barua hiyo inanukuu
baadhi ya maneno yaliyosemwa na Mwakibinga dhidi ya Dk. Nchimbi,
yakiwemo haya; “kuna mtandao wa wezi na wabadhirifu wa mali za UVCCM
unaofanywa na vijana pamoja baadhi ya watendaji, na ujangili huu
unaaanzia katika Baraza la Wadhamini.”
Huku ikieleza kuwa,
maneno yaliyosema na Mwakibinga yalilenga kuonyesha Dk.Nchimbi ni mwizi,
jangili, hatari, asiyefaa kuwa kiongozi na asie na maadili na
inahitimisha kwa kusema;
“Kutokana na sababu
tulizotaja, tumeelezwa na mteja wetu kwamba, uchukue kila hatua
itakayosafisha jina lake hasa kwa kuitisha mkutano mwingine na
wanahabari mara moja na ukanushe tuhuma ulizotoa na kuomba radhi.
Pia ufute na kuondoa
taarifa iliyomkashifu katika vyombo vyote vya habari pamoja na mitandao
ya kijamii na umlipe haraka iwezekanavyo mteja wetu fidia ya shilingi
2.5 bilioni.
Wakati Dk. Nchimbi
akikusudia kumshitaki Mwakibinga, itakumbukwa kuwa, kijana huyo
alipoitisha mkutano na wanahabari alidai kuwa anao ushahidi wote dhidi
ya tuhuma alizozitoa na aliahidi kuweka wazi ushahidi huo iwapo
watuhumiwa wangekanusha.
Dk. Nchimbi amewahi kuwa
waziri katika serikali ya awamu ya nne, akihudumu katika wizara mbili
tofauti katika kipindi cha zaidi ya miaka nane, lakini pia amekuwa
Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Ruvuma kwa kipindi cha miaka 10.

No comments:
Post a Comment